Mahakama ya juu ya Niger siku ya Ijumaa iliondoa kinga ya rais Mohamed Bazoum, na hivyo kutoa fursa kwa kesi inayowezekana juu yake baada ya kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi ya Julai 2023.
“Mahakama inaamuru kuondolewa kwa kinga ya Mohamed Bazoum,” ilisema chombo hicho, iliyoundwa mnamo Novemba na uongozi mpya wa kijeshi. Mamlaka ya Niger inamshutumu Bazoum kwa uhaini, kufadhili ugaidi na kupanga njama ya kuhujumu serikali.
Bazoum amezuiliwa katika makazi ya rais tangu Julai mwaka jana, wakati maafisa wa jeshi la Niger walipopindua serikali yake katika mapinduzi ya kijeshi.
Mnamo Agosti, mamlaka ya kijeshi ilitangaza mipango ya kumshtaki kwa “uhaini mkubwa” na kudhoofisha usalama wa taifa.
Mnamo Aprili, mamlaka ilianzisha kesi za kisheria dhidi yake ili kuondoa kinga yake ya urais ili aweze kufunguliwa mashtaka kwa madai ya uhalifu uliofanywa baada ya kuchaguliwa kuwa rais mnamo 2021.