Mahakama ya Misri imekataa ombi la mmiliki wa meli ya Ever Given ambayo ilizuia njia ya Mfereji wa Suez mwezi Machi wa kutaka meli hiyo iachiwe huru.
Mmiliki wa meli hiyo, Shoei Kisen aliiomba mahakama hiyo itoe amri ya kuachiwa huru kwa meli hiyo inayoshikiliwa na mamlaka ya ya Mfereji wa Suez inayotaka kulipwa fidia ya dola za Marekani milioni 916 (zaidi ya trilioni 2 za Tanzania).
Mamlaka ya usimamizi wa Mfereji wa Suez inasema fidia hiyo inajumuisha gharama za kuinasua meli hiyo kutoka kwenye matope na hasara ya kushindwa kutoa huduma kwa meli na vyombo vingine vya baharini kwa siku sita na [vyombo hivyo] kulazimika kutafuta njia nyingine kufuatia njia ya mfereji huo kuzibwa na Ever Given.