Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza limerejeshewa umiliki wa kiwanja namba 111 kitalu (T) kilichopo Barabara ya Kenyatta eneo maarufu la Stendi ya Igombe, kilichokuwa chini ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
BAKWATA wamerejeshewa eneo hilo baada ya kushinda kesi dhidi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya Halmashauri hiyo kushindwa kutimiza masharti waliyopewa na Mahakama.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema katika maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ilitoa masharti mawili kwa Halmashauri ya Jiji ikitakiwa kulipa fidia ili kumiliki eneo hilo au irudishe eneo kwa Mmiliki halali kama fidia ndani ya miezi mitatu, ambapo Halmashauri ilishindwa kutekeleza yote mawili.
Shauri hilo namba 150 la mwaka 2020 lililotokana na kesi namba 58 ya mwaka 2017 liliamuliwa June 3, 2022, ambapo kwa mujibu Mahakama ilithibitisha kwamba kiwanja hicho ni mali halali ya Baraza la Waislamu Tanzania.