Mahakama nchini Rwanda imetupilia mbali rufaa ya kiongozi mashuhuri wa upinzani kutaka hukumu yake ya awali iondolewe, na hivyo kumnyima sifa ya kumpinga Rais Paul Kagame katika uchaguzi wa mwezi Julai.
Bernard Ntaganda, mwenye umri wa miaka 55, mkosoaji mkali wa mtawala wa Rwanda aliyetumia mkono wa chuma, aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu mjini Kigali mwezi Februari kwa nia ya kufuta hatia zilizokuwepo tangu zaidi ya muongo mmoja.
Ni kiongozi wa pili wa upinzani kuzuiwa kugombea katika uchaguzi wa Julai 15 dhidi ya Kagame, ambaye anatarajiwa kushinda kwa muhula wa nne wa miaka saba madarakani.
Jopo la majaji watatu lilitoa uamuzi dhidi ya Ntaganda, kutokana na kile ilichosema ni kushindwa kulipa ada ya mahakama ya karibu faranga 106,000 za Rwanda (kama dola 82) zinazohusiana na kesi ya awali dhidi yake.