Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha miaka 5 jela ama kulipa faini ya Tsh. Milioni 10, washtakiwa watatu baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha wasichana 10 kwenda Kenya ili wakajishughulishe na biashara ya ngono.
Mbali na adhabu ya kifungo, pia Mahakama hiyo imetaifisha simu mbili zilizokuwa zikitumiwa na washtakiwa kwa kuziharibu mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Jackline Milinga, Simon Mgaya wote raia wa Tanzania na Mary Amukowa ambaye ni raia wa Kenya.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa alisema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi 12 wa upande wa mashtaka.
>>>”Washtakiwa mmekutwa na hatia, hivyo mtalipa faini ya Tsh Milioni 10 kila mmoja au kwenda jela miaka mitano kila mmoja.”
Hakimu Mwambapa alisema kuwa washtakiwa walikamatwa katika mpaka wa Namanga, wakiwa na wasichana hao, baada ya kubainika kuwa hawakuwa na hati za kusafiri kutoka Tanzania kwenda Kenya.
Hakimu Mwambapa alisema kuwa mshtakiwa wa Jackline na Mary walihusika kuwatafuta wasichana hao wenye vigezo vya urembo na kuwakatia tiketi wakati Simon alihusika kuwatafutia taksi ya kuwatoa Makumbusho hadi katika basi la Modern Coach.
Awali, Wakili wa Serikali Estazia Wilsoni aliomba Mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao ili iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama yao.>>>”Kupitia kifungu namba 351(i)cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, tunaomba amri ya Mahakama ya kutaifisha simu mbili zilizotumiwa na washtakiwa hao katika kufanikisha usafirishaji wa mabinti hawa.”
Hata hivyo washtakiwa walipopewa nafasi ya kujitetea kwa nini wasipewe adhabu ambapo waliomba Mahakama iwahurumie kulingana na umri wao kwa sababu wamekaa gerezani miaka miwili, huku mshtakiwa Simon akidai kuwa yeye ana familia ya mke na mtoto mchanga.
Katika kesi hiyo, Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa, Septemba 4, 2015 katika eneo la Magomeni na Makumbusho wanadaiwa kusafirisha wasichana 10 wenye umri chini ya miaka 20 kutoka Tanzania kwenda Nairobi nchini Kenya, kwa ajili ya kuwafanyisha biashara ya kingono
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwasafirisha mabinti 10 kutoka Tanzania kwenda Kenya ambao ni Najma Suleimani, Leah Musa, Zulfa Ally, Rahma Mohamed, Salima Komba, Angelina Banzi, Leila Chorobi, Elizabeth Nalimu, Amina Abdi na Sada Husein.
Video iliyomnasa Gwajima akiondoka Mahakamani baada ya kuachiwa huru
Video ikimuonyesha Yusuf Manji akiondoka Mahakamani baada ya kuachiwa huru