Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda ahakikishe anawakamata viongozi wa AMCOS kwa tuhuma za kutoa fedha za wanachama na kuwapa madiwani ili wakawashawishi madiwani wenzao wakubali kubadilisha eneo la ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Madiwani waliohusika katika mvutano huo ni wa kata za Mkumbi (Bruno Kapinga), kata ya Lukalasi (Bosco Ndimbo) na wa kata ya Linda (Haule), ambao wanadaiwa kuchukua fedha kutoka kwa watendaji wa AMCOS kwa ajili ya kwenda kushawishi madiwani wenzao wakubali kuhamishwa kwa eneo la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo.
Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme asimamie ujenzi wa halmashauri hiyo unaoendelea katika eneo la Kigonsera.
Mvutano huo unaongozwa na Madiwani hao wa Kata tatu za Mkumbi, Lukalasi na Linda ambao wanataka makao makuu yajengwe kwenye kata ya Mkumbi katika eneo ambalo litailazimu Serikali ilipe fidia ya zaidi ya Sh milioni 400 huku kukiwa na eneo la bure la ekari 150 ambalo ndiko yanakojengwa makao makuu.
“Hatuwezi kukubali huko mnakotaka nyie ni lazima tulipe fidia ya zaidi ya Sh milioni 400 na kuna eneo la bure ekari zaidi ya 150, hii haikubaliki hatuwezi kufanya mambo kama haya kwenye fedha za wananchi haiwezekani. Mmeamua kila AMCOS ichange Sh 600,000 mpate milioni tatu mfanye kampeni ya kutaka halmashauri ijengwe kwenye eneo lao hiyo ni rushwa” Majaliwa
“Kwa kuwa zile ni fedha za wakulima, Kamanda wa TAKUKURU kawakamate watendaji wa AMCOS hizo wahojiwe kwa nini walitumia fedha za kuwapa Madiwani wakahonge ni lazima wahojiwe waeleze ni nani aliyetoa maagizo ya kutoa Sh milioni tatu,” Majaliwa.