Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametembelea banda la Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwenye maonesho ya madini kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIF) na kuipongeza kampuni hiyo kwa kutekeleza kikamilifu mpango wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).
Majaliwa ambaye pia juzi Alhamisi alifunga mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, alipata maelezo kutoka kwa Meneja Mwandamizi anayeshughulikia mahusiano ya jamii kutoka GGML, Gilbert Mworia na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na kampuni hiyo ikiwemo kuwa mdhamini mkuu wa mkutano huo.
“Tunawapongeza sana kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuzingatia matakwa ya sheria ya madini kuhusu kipengele hicho cha CSR, kwa mfano katika hili suala la ujenzi wa uwanja wa mpira Magogo mnatakiwa kumalizia kulitekeleza haraka ndani ya miezi sita.
“Lakini pia msiangalie kujenga uwanja mkoani Geita peke yake, mmpeleke huduma hizi na mikoa mingine ili ifaidike na kukuza vipaji vya vijana wetu,” alisema Majaliwa.
Awali akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Meneja huyo Mwandamizi mbali na kuelezea mikakati ya GGML katika kuhakikisha watanzania na jamii inayozunguka mgodi inanufaika na uwepo wa GGML, pia alisema kampuni hiyo imekuwa kinara katika kuzingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira, afya na usalama mahala pa kazi.
Mworia alisema GGML imeendelea kuwa mfano wa kuigwa nchini kutokana na kuzingatia suala la afya na usalama mahala pa kazi hali iliyoifanya kampuni hiyo kushinda mara nne mfululizo tuzo hiyo inayotolewa na kampuni mama ya AngloGold Ashanti na kuishinda migodi mingine duniani.
Kuhusu ujenzi wa uwanja huo wa mpira, Mworia alimhakikishia waziri mkuu kuwa ndani ya miezi sita utakuwa umekamilika lakini pia wataandaa mpango wa kutoa mchango katika sekta hiyo kwenye mikoa mingine.
Hata hivyo, akifunga maonesho hayo yaliyofanyika tarehe 25, 26 Oktoba mwaka huu, Majaliwa alisema Serikali itaendelea kuipa umuhimu sekta ya madini ilikuwa injini ya uchumi wa Taifa.
Alisema Serikali ipo tayari na inaruhusu miradi ya maendeleo kutoka Sekta binafsi katika Utafutaji, Uchimbaji, uchorongaji na uongezaji thamani madini ili kufanikisha mikakati iliyopo kwa wachimbaji kwa wachimbaji wote nchini.
Naye Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema wizara imetumia mkutano huo katika kukuza ushirikiano wa kikazi baina ya nchi na nchi kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa kama vile majadiliano kuhusu matumizi ya nishati safi ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema kwa mwaka 2023 mchango wa wachimbaji katika sekta madini ilikusanya Sh bilioni 678 sawa na asilimia 40 ya makusanyo yote hali inayoonesha sekta hiyo kupiga hatua.