Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 na 2023/2024 Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 11.15 kwa ajili ya ununuzi wa magari 65 na kuendeleza ujenzi wa majengo ya magereza kwenye mikoa ya Morogoro, Kigoma, Arusha, Tabora, Dodoma na Pwani.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Desemba 15, 2023), wakati akifunga Mafunzo ya Juu na Daraja la Pili kwa Askari wa Jeshi la Magereza, katika Chuo cha Mafunzo cha Magereza Ukonga (TCTA), ambapo ametumia fursa hiyo kuwataka wahitimu hivyo basi wote wakazingatie mafunzo waliyoyapata ili yakawe chachu katika kuboresha utendaji kazi wa majukumu yao ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Serikali imelipatia Jeshi la Magereza magari kwa ajili ya shughuli za utawala na usafirishaji wa mahabusu, hadi kufikia tarehe 22 Mei, 2023 tayari Serikali ilikuwa imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 4.459 kwa ajili ya ununuzi wa magari 23, kati ya hayo, magari 18 ni ya utawala na matano ya mahabusu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha Jeshi la Magereza limetengewa shilingi bilioni 6.691 kwa ajili ya ununuzi wa magari mengine 42 yatakayotumika kwa shughuli za utawala na utekelezaji wa jukumu la usafirishaji wa mahabusu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.769 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Magereza ya Gairo na Kilosa Mkoani Morogoro, Kakonko mkoani Kigoma, Kaliua na Igunga Mkoani Tabora, Karatu Mkoani Arusha, Msalato na Isanga Mkoani Dodoma, na Gereza la Kwa Mturuki lililopo Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani.
Amesema miradi hiyo inatekelezwa sambamba na kuanza ujenzi wa magereza mapya ya Kiabakari Mkoani Mara, Mpimbwe katika Mkoa wa Katavi, Sengerema Mkoani Mwanza, Kyerwa Mkoani Kagera, Kingurungundwa Mkoani Lindi na Gereza la Mlolo lililoko Mkoani Iringa.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Ofisi za Magereza katika Mikoa ya Geita, Kigoma, Lindi, Songwe na Tanga pamoja na shilingi milioni 225 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba za maafisa na askari wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani zilizopo Msalato Mkoani Dodoma.
“Licha ya hayo, Serikali imetenga shilingi milioni 285 kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama katika magereza matano. Magereza hayo ni Ilagala lililoko Mkoani Kigoma, Mbarali Mkoani Mbeya, Kiteto katika Mkoa wa Manyara, Kingurungundwa Mkoani Lindi na Gereza la Kongwa Mkoani Dodoma.” Amesema kukamilika kwa miradi hiyo ya ujenzi kutahakikisha uwepo wa huduma bora, mazingira bora ya kazi, makazi bora na mahali salama pa kuhifadhi wafungwa na mahabusu.