Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limelaani idadi “ya kushangaza” ya watoto waliopoteza maisha huko Gaza, ambapo maafisa wanasema mashambulizi ya Israel yameua zaidi ya watoto 2,000.
Ikiripoti kuwa watoto 2,360 wameuawa katika muda wa chini ya wiki tatu, UNICEF imetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na upatikanaji endelevu na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu.
Watoto wengine 5,364 huko Gaza wamejeruhiwa katika “mashambulizi yasiyoisha,” UNICEF iliongeza Jumanne. Zaidi ya watoto 400 wanaripotiwa kuuawa au kujeruhiwa kila siku katika eneo la Palestina lililozingirwa, ilisema.
Tarehe 7 Oktoba kundi la Hamas la Palestina lilianzisha mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya Israel na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,400.
Jeshi la Israel tangu wakati huo limeshambulia kwa mabomu Gaza na kuua takriban watu 5,791. Watoto ni takriban asilimia 50 ya wakazi wa Gaza wapatao milioni 2.3.
“Hali katika Ukanda wa Gaza ni doa inayoongezeka kwenye dhamiri zetu za pamoja. Kiwango cha vifo na majeraha ya watoto kinashangaza tu,” alisema Adele Khodr, mkurugenzi wa UNICEF wa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
UNICEF imesema watoto 30 waliripotiwa kuuawa katika ghasia za hivi majuzi nchini Israel, huku makumi ya watu wakiwa bado mateka ndani ya Gaza baada ya Hamas kuwateka takriban watu 220.