Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Dar es Salaam (DAWASA) imewahakikishia wananchi wanaohudumiwa na Mtambo wa Ruvu chini kuwa huduma ya maji itarejea ndani ya muda uliopangwa kufuatia matengenezo ya bomba kubwa la inch 54 lililopo eneo la Mlalakuwa, Mwenge kuendelea kutengenezwa kwa kasi inayoridhisha.
Akielezea juu ya matengenezo hayo Meneja Uzalishaji na Usambazaji wa maji, DAWASA Mhandisi Tyson Mkindi amesema mafundi wanaendelea na matengenezo ambayo kwa sasa yamefikia asilimia 60, na kwamba huduma ya maji itarejea ndani ya muda uliopangwa na Mamlaka.
“Kazi inaendelea baada ya kuanza tangu saa mbili asubuhi na mpaka sasa (saa 10:13 asubuhi) tumefikia asilimia 60 ya utekelezaji, hivyo tunatarajia huduma kurejea kabla ya wakati tulioutegemea kwa kuwa hamna changamoto yoyote iliyojitokeza mpaka wakati wa utekelezaji,” amesema Mhandisi Mkindi.
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Mlalakuwa, Ndugu *Suleiman Massare* amesema kuwa wamejiridhisha na jitihada zinazofanywa na DAWASA katika eneo lake amewataka wakazi wa mtaa wake na waliathirika na matengenezo hayo kuwa na subira kwa kuwa matengenzo yanatarajiwa kukamilika leo jioni.
“Kazi inayoendelea hapa inatia moyo kuwa huduma itarejea ndani ya muda uliopangwa, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi,” amesema Ndugu Massare.
Matengenezo ya bomba kubwa la maji eneo la Mlalakuwa limepelekea kuzimwa kwa mtambo wa Ruvu chini na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es salaam kuanzia Mji wa Bagamoyo hadi katikati ya Jiji kwa maeneo ya Ilala hadi Kigamboni.