Kutokana na historia ya matukio ya kutokuwa na maelewano mazuri baina ya wafugaji na wakulima katika mkoa wa Morogoro na wilaya zake, Jumapili ya October 16, 2016 imemfikisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano January Makamba ambaye amekutana na kuzungumza na wakazi wa kijiji cha Mbwade, Kata ya Madoto, Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwa jamii.
Waziri Makamba akiwa na viongozi wa wilaya na mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoi, ambaye amesikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho ambacho kinakaliwa na wakulima na wafugaji ambapo kwa kiasi kikubwa wameeleza changamoto kubwa ya mgawanyo bora wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji hasa katika kipindi cha ukame kuanzia mwezi wa 9, 10 na 11 ambacho kimetajwa kuwa na migogoro sana.
Baada ya mkutano na pande zote mbili, Waziri January Makamba ametoa maagizo matano ambayo yanatakiwa kutekelezwa kabla ya mwisho wa mwezi November 2016. Maagizo hayo ni kama ifauatavyo.
- Kamati ya Amani ya Kijiji Cha Mbwade na Kijiji Cha Parakuyo itakayochaguliwa, kuheshimiwa na kuaminiwa na wananchi ambayo itasuluhisha migogoro ya mara kwa mara inayojiyokeza kati ya wakulima na wafugaji. Waziri Makamba ataziwezesha Kamati hizo kupata uwezo wa tasnia ya kusuluhisha migogoro inayotokana na ufinyu wa rasilimali. Hata hivyo, sheria itachukua mkondo wake kwa wale watakaovunja amani kwa kisingizio cha kutafuta malisho au kuchepusha mto kwa kilimo.
- Kuundwe Kamati za Mazingira Kwa kila kijiji (kama ambavyo Sheria ya Mazingira inataka). ambapo yeye kama Waziri mwenye dhamana ameahidi kuziwezesha Kamati hizo kwa mafunzo ya hifadhi ya Mazingira ili ziweze kuwafundisha wanavijiji wote (wakulima na wafugaji) kuhusu hifadhi ya mazingira.
- Vijiji vitengeneze Sheria Ndogo za Vijiji za Mazingira na Sheria hizo zitekelezwe kwa ukamilifu.
- Serikali itatengeneza mradi mahsusi wa kusaidia jamii kukabiliana na athari ya Mabadiliko ya Tabianchi (Climate Change Adaptation).
- Ombi la jamii za wafugaji na wakulima kuongezewa maeneo mapya litazingatiwa tu na Serikali pale ambapo jamii hizo zitakubali kufanya uhakiki wa idadi ya mifugo yao na pia kutoruhusu wafugaji kutoka maeneo mengine kuhamia na mifugo mipya katika maeneo hayo.
Katika ziara hiyo, Waziri Makamba alifika katika kijiji cha Twatwatwa kata ya Parakuyo na kujionea changamoto wanazokumbana nazo wafugaji hasa kipindi cha kiangazi na kuwaasa wananchi hao kushiriki katika zoezi la uhakiki wa mifugo ili kurahisishia kuweka mipango sahihi ya kuwasaidia, huku akisisitiza juu ya matumizi bora ya ardhi kwa wakulima na wafugaji.
UMEPITWA NA UCHAMBUZI WA MAGAZETI YA LEO OCTOBER 17? NIMESHAKUWEKEA HAPA