Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere amesema alichaguliwa kuwa mbunge wa Arusha mwaka 1995 kwa uwezo wake si kubebwa kwa sababu ni mtoto wa rais mstaafu, Hayati Julius Nyerere.
Ameyasema hayo Mjini Babati katika makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti ambaye amehamishiwa Mkoa wa Rukwa.
Makongoro amesema alikuwa mkazi wa Arusha wakati huo alipochaguliwa kuwa mbunge kwa tiketi cha chama cha NCCR-Mageuzi, “Arusha walikuwa wananiita Chamaa kwa sababu niliishi nao vizuri wakanichagua ili niwe mwakilishi wao na sio kama baadhi ya watu wanavyodai kuwa nilichaguliwa kwa sababu ni mtoto wa baba wa Taifa.”
Kuhusu utendaji kazi katika Wilaya hiyo, amewataka viongozi mkoani humo kutowanyanyasa watumishi na wananchi kwa kuwa hatokubali kuona mnyonge akionewa kwenye eneo hilo.
“Wakuu wa wilaya pambaneni na migogoro ya ardhi, mfano hapa Babati nimefika na kukuta kuna mama mjane analalamikia kunyang’anywa eneo lake na watu wenye fedha kisha wanamwambia aende mahakamani,” Makongoro.