Mali imesisitiza kuwa haitasalia kimya iwapo wanajeshi wa kigeni, kuna Jumuiya ya nchi za ECOWAS, itaivamia Niger, kumrudisha madarakani rais aliyepinduliwa mwezi Julai, Mohamed Bazoum.
Waziri wa Mambo ya nje wa Mali, Abdoulaye Diop, ametoa kauli hiyo wakati akitoa hotuba kwa niaba ya uongozi wa kijeshi kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, jijini New York.
Diop amesema jaribi lolote la kuishambulia, Niger, litakuwa tishio la amani kwa Mali na ukanda wote, na Bamako haitasalia kimya iwapo jirani yake ya Niger, itavamiwa.
Mali imetoa kauli hii baada ya wiki moja iliyopita, kuingia kwenye mkataba wa ushirikiano wa kijeshi pamoja na Niger na Burkina Faso, ambazo zinaoongozwa na jeshi tangu mwaka 2020.
Jumuiya ya ECOWAS inasema, bado nia ya kutumia jeshi nchii Niger ipo lakini kwa sasa, jitihada za kidiplomasia zinaendelea, kati ya jumuiya hiyo na wakuu wa jeshi, kwa mujibu wa rais wa Senegal Macky Sall, alipozungumza na RFI wiki hii.