Raia 49 na wanajeshi 15 wameuwawa nchini Mali jana usiku baada ya shambulio la boti linalohusishwa na wanamgambo wa kislamu.
Kulingana na taarifa ni kuwa boti hilo lilishambuliwa lilipokuwa likisafiri kutoka Gao na kunao raia waliojeruhiwa vibaya na huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.
Washambuliaji hao pia walivamia kambi ya kijeshi katika eneo la Bourem Circle, lililoko katika jimbo la Gao, kaskazini mashariki mwa Mali. Takriban washambuliaji 50 waliuawa katika makabiliano, na siku tatu za maombolezo ya kitaifa zilitangazwa, ilisema serikali ya mpito.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa likipambana na vuguvugu la wanajihadi lenye mafungamano na lile la Al-Qaeda na kundi la Islamic State kwa takriban muongo mmoja.
Wanajihadi na wapiganaji wanaotaka kujitenga baadhi wakiwa na mfungamano na Al-Qaeda na kundi la Islamic State walianza operesheni nchini Mali mwaka 2012 na mzozo huo umeenea hadi nchi jirani za Niger na Burkina Faso, na kuua na kuwafukuza maelfu ya raia.