Klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imetwaa ubingwa wa Kombe la Ligi ya Kandanda ya Afrika baada ya kuicharaza Wydad Casablanca jumla wa mabao 3-2 kwenye fainali ya mkondo wa pili iliyopigwa Jumapili hii ya Novemba 12.
Fainali ya kwanza iliishuhudia Wydad ikishinda mabao 2-1 nyumbani katika Uwanja wa Mohamed V, Morocco, kabla ya Sundowns kushinda mabao 2-0 wakiwa nyumbani pia katika Uwanja wa Loftus Versfeld, mjini Pretoria.
Mabao ya Sundowns kwenye fainali hiyo ya kukata na shoka yalifungwa na Peter Shalulile kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza, na Aubrey Modibe kunako dakika ya 53.
Waafrika Kusini hao wameandika historia kuwa klabu ya kwanza kutwaa kombe la ligi hiyo mpya ya African Football League iliyozinduliwa msimu huu.
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Kandanda Afrika CAF, Patrice Motsepe ni miongoni mwa shakhsia watajika waliokuwa uwanjani mjini Pretoria kushuhudia fainali hiyo.
Klabu ya Mamelodi imeondoka na kitita cha Dola za Kimarekani Milioni 4 kwa ushindi huo.