Shirika la Afya Duniani, WHO limesema Jumanne kwamba limeweza kuendesha kampeni ya utoaji wa chanjo za polio katikati mwa Gaza kwa maelfu ya watoto licha ya mashambulizi ya Israel kwenye maeneo maalum yaliyotengwa saa chache kabla ya mashambulizi hayo.
Kama sehemu ya makubaliano kati ya Jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas, sitisho la mapigano kwa muda, kwa misingi ya kibinadamu kwenye mapigano hayo yaliyochukua mwaka mmoja lilikuwa lianze Jumatatu, ili kufikia mamia ya maelfu ya watoto walioathiriwa.
Hata hivyo saa chache kabla ya hilo kufanyika, maafisa wa misaada wa Umoja wa Mataifa walisema kuwa vikosi vya Israel vilishambulia mahema kadhaa karibu na hospitali ya Aqsa, iliopo kwenye sehemu maalum iliotengwa, ambapo watu wanne walipoteza maisha.
Shirika la UN kwa ajili ya Palestina la UNRWA limesema kuwa moja ya shule kwenye mji wa kati kati mwa Gaza wa Nuseirat, ambayo ilitengwa kama sehemu ya kutolea chanjo ilishambuliwa usiku kucha kati ya Jumapili na Jumatatu, na kuuwa watu 22.