Mamlaka nchini Somalia imepiga marufuku uvaaji wa barakoa katika mji mkuu, Mogadishu, kutokana na hofu ya kiusalama.
Msemaji wa utawala wa Mogadishu, Salah Dheere, alisema kuwa uvaaji wa barakoa ulikuwa unatumika kuficha utambulisho na kurahisisha vitendo vya uhalifu.
Barakoa hizo zilitumika sana wakati wa janga la Covid-19.
Mamlaka pia iliharamisha uvaaji wa kofia na kubeba silaha katika usafiri wa umma.
Hata hivyo, kofia za jadi za sunna zinazovaliwa na wazee haziruhusiwi kupigwa marufuku.
Uamuzi huo ulitolewa wakati wa mkutano wa hivi majuzi wa usalama mjini Mogadishu, ulioongozwa na Rais Hassan Sheikh Mohamud.
Somalia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi, huku vitisho vikuu vikitoka kwa kundi la wanamgambo wa al-Shabab.