Mamlaka nchini Uganda imeripotiwa kusitisha marufuku ya hivi majuzi ya uuzaji wa nyama katika mji mkuu wa Kampala, huku kukiwa na mlipuko wa ugonjwa wa mifugo.
Maafisa wa afya walikuwa wametangaza marufuku hiyo wiki jana na kuamuru kufungwa kwa maeneo yote ya vichinjio kupunguza kuenea kwa mlipuko huo.
Waziri wa masuala ya jiji la Kampala Minsa Kabanda, hapo jana Jumapili aliliambia gazeti la Daily Monitor la nchini humo kwamba marufuku hiyo imesitishwa huku serikali ikiendelea kutathmini athari za ugonjwa huo katika mji mkuu.
Kabanda hata hivyo aliwataka watu kuhakikisha kuwa mifugo wamepimwa kabla ya kuchinjwa.
Wafanyabiashara walikuwa wamepinga marufuku hiyo na kuishutumu serikali kwa kushindwa kuzuia ugonjwa huo kuenea.
Ugonjwa huo wa mifugo umeripotiwa katika wilaya 40 kote nchini, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.