MAMLAKA na taasisi mbalimbali za Serikali zinatarajiwa kutumia maonesho ya magari ya Isuzu jijini Dodoma kupata elimu kuhusu teknolojia za kisasa zinazotumika katika kuandaa magari mbalimbali.
Maonesho hayo pia yanalenga kutoa suluhisho mbalimbali za usafiri kupitia kampuni ya magari ya Isuzu yaliyoundwa yakilenga kuboresha utoaji wa huduma nchi nzima hususani kwa serikali na Mamlaka zake pamoja na matumizi binafsi.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi tarehe 13 Februari, 2025 na Meneja Mkuu wa kampuni ya Al Mansour Auto EA Tanzania, Anurup Chatterjee katika uzinduzi wa maonesho hayo yanayoendelea katika viunga vya jengo la Akachube Plaza, lililopo kando ya Shoppers Plaza jijini Dodoma.
Maonesho hayo yanayoratibiwa na Kampuni ya Al Mansour Auto EA Tanzania, ambao ni wauzaji na wasambazaji wa magari aina ya Isuzu nchini, yanafanyika kwa siku ya tatu ya magari hayo jijini Dodoma.
Alisema maonesho hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa Februari 14 mwaka huu, yanalenga kuboresha sekta ya usafirishaji na uchukuzi nchini kwa kutambulisha teknolojia za kisasa kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo muhimu kiuchumi.
“Wananchi na wadau mbalimbali wanaoendelea kutembelea maonyesho haya watapata fursa ya kuchunguza na kujionea aina mbalimbali ya magari ya kibiashara ya ISUZU, ikiwa ni pamoja na malori, mabasi na magari madogo (pick-ups, na SUV) ambayo yanajulikana kwa uimara na kutegemewa katika sekta mbalimbali kama vile miradi ya miundombinu ya umma, operesheni za usalama, miundombinu ya usafiri kwenye sekta ya kilimo, na huduma muhimu katika sekta za afya na elimu.,” alisema.
Kwa ajili ya shughuli za ‘field’ na usafiri wa kiutawala, kupitia maonesho hayo, kampuni hiyo imejipanga kuonesha magari ya ISUZU D-MAX pick-ups katika mipangilio ya Single Cab na Double Cab, ambayo ni bora kwa mashirika ya serikali, programu za kufikia maeneo ya vijijini, na kazi zinazoenda nje ya barabara.
“Tupo hapa pia kuionyesha gari aina ya ISUZU SUV yenye viti 7 (mu-X) kama chaguo imara na lenye uwezo wa juu kwa matumizi rasmi na binafsi,” aliongeza.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Meneja wa Masoko ya Nje wa Kampuni ya Isuzu Afrika Mashariki, Sandra Njagi pamoja na kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuunga matumizi ya magari hayo hususani magari makubwa, aliomba kasi hiyo ielekezwe zaidi pia kwenye magari madogo ambayo pia yameundwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko la Tanzania ikiwemo barabara za pembezoni pamoja na gharama rafiki.
“Hata hivyo, kiasi kikubwa tunaridhishwa na ushirikiano tunaoendelea kuuhushudia kati yetu sisi kama Isuzu na serikali ya Tanzania na hiyo ndio sababu tumeamua kusogeza huduma zetu pia hadi hapa Dodoma ili tuendelee kuwa karibu na wateja wetu hususani mamlaka mbalimbali za serikali. Kama ambavyo wamekuwa wakituunga mkono kwenye magari makubwa ndivyo pia tunalenga kuwaonesha pia tunayo magari madogo pia yanayofanya vizuri zaidi,” alisema.
Kwa upande wake Msimamizi Mwandamizi wa Masoko wa Kampuni ya ya Al Mansour Auto EA Tanzania, Catherine Mwera alisema tangu kuanza shughuli zake mwezi Julai 2020, kampuni hiyo imeshuhudia ukuaji mkubwa katika sekta ya magari, ikijijengea jina kama msambazaji mkuu wa magari ya ISUZU kwa wateja serikali na sekta binafsi nchini.
“Uamuzi wetu wa kuja Dodoma yalipo makao makuu ya serikali kwa kiasi kikubwa umechochewa na ushirikiano mkubwa wa kibiashara tunaoupata kutoka kwa wateja wetu muhimu kutoka serikali wakiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais Zanzibar na mashirika mengi binafsi,” alitaja.