Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini (DCEA) imejikita kudhibiti matumizi ya dawa hizo mitaani baada ya kuibuka matumizi mengine ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kuanza kutumiwa Kwa kiwango cha juu kama mbadala wa Dawa za Kulevya.
Akizungumza kwenu kikao cha kuwajengea uelewa watendaji wa kata na mitaa katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza Afisa Elimu kwa umma kutoka DCEA, Dezidel Tumbu amesema matumizi ya dawa hizo yapo katika kiwango kikubwa ambapo waraibu wanalazimika kutumia kama mbadala wa Dawa za Kulevya.
Tumbu ameeleza pia katika mikoa hiyo ya kanda ya Ziwa kuna matumizi makubwa ya dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi ambayo mara kadhaa wamekuwa wakiikamata mashambani.
Akizungumzia changamoto hiyo, Afisa Sheria Mkuu DCEA, Christina Rweshabura amesema katika kipindi cha muda mfupi wamefanikiwa kukamata watu 11 waliokuwa wanajihusisha na kusafirisha bangi, pia walifanikiwa kukamata magunia 507 ya bangi kavu na gunia 50 za mbegu aina ya bangi.
Amesema kupitia sheria ya kupambana na kudhibiti dawa za kulevya sura ya tano mtu atakayebainika na dawa za kulevya kuanzia kilo 100 atahukumiwa kifungo cha maisha jela.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho, Praxeda Ngozi amesema elimu hiyo imewaongezea uelewa wa kubaini viashiria vya uwepo wa matumizi ya dawa kwenye maeneo yao tofauti na awali ambapo hawakuwa wanaelewa.