Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza kufuta ratiba za saa tisa alfajiri na saa kumi na moja alfajiri kwa mabasi 38 ya New Force Enteprises ( mabasi 10 ni yale yanayoanza safari saa tisa alfajiri na mabasi 28 yanayoanza safari saa kumi na moja alfajiri) kufuatia mfululizo wa ajali za mabasi hayo ambapo ndani ya wiki nne kati ya June 06 – July 02,2023 mabasi matano yamepata ajali.
“Kuanzia tarehe 5 Julai, 2023 mabasi haya 38 yatafanya safari zake kuanzia saa 12.00 asubuhi na kuendelea hii ni kwakuwa uchunguzi wa awali wa LATRA ulibaini kuwepo kwa uvunjaji wa makusudi wa kanuni hususani kutumia ratiba za saa 9.00 alfajiri na saa 11.00 alfajiri bila dereva kuwa amethibitishwa na LATRA na pengine dereva kuwa amethibitishwa lakini hatumii mfumo wa utambuzi wa dereva (i-button) anapoendesha basi”
“Kanuni zinamtaka dereva anayeendesha basi la abiria kutumia kifaa cha utambuzi ili tuweze kuwafuatilia kwa mfumo wetu wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) yanapokuwa safarini lakini uchunguzi tulioufanya kwenye magari haya yaliyopata ajali tumebaini ukiukwaji wa sharti hilo kwa mabasi ya Kampuni ya New Force Enterprises”
“Kutokana na ukiukwaji huu, Mamlaka imeshindwa kuwatambua madereva waliokuwa wanaendesha mabasi haya ili kuweza kuwachukulia hatua au kupeleka taarifa zao Jeshi la Polisi – Kikosi cha Usalama Barabarani ili wawajibishwe kwa mujibu wa Sheria za Usalama Barabarani, pia tumebaini ukiukwaji wa ratiba za mabasi ambayo hayakuwa kwenye ratiba ya saa 9.00 alfajiri na saa 11.00 alfajiri kwa kufanya safari muda huo bila kibali cha LATRA”