Wanaharakati wa haki za binadamu Jumatatu walishutumu mamlaka ya Belarus kwa kuweka masharti yasiyokubalika ya kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuandika taarifa za umma kukiri hatia yao na kutubu.
Shutuma hiyo inajiri siku chache baada ya Rais Alexander Lukashenko kuahidi kuwaachilia wale ambao ni wagonjwa mahututi na wale waliofagiliwa wakati wa maandamano makubwa ya 2020 dhidi ya utawala wake.
Idadi ya walioachiliwa hadi sasa imefikia angalau 18, kulingana na wanaharakati, miongoni mwao kiongozi wa chama cha upinzani Ryhor Kastusiou ambaye anaugua aina kali ya saratani. Marekani na Umoja wa Ulaya wamekaribisha kuachiliwa kwa baadhi ya wafungwa wa kisiasa lakini wametoa wito kwa Belarus kuwaachilia wale wote waliofungwa jela wakati wa maandamano ya 2020.
Baadhi waliachiliwa kwa msamaha huku wengine wakisamehewa. Wale waliosamehewa walipaswa kukiri hatia yao hadharani. Baadhi ya wafungwa wa kisiasa wamekataa kuandika barua kama hiyo kwani hawaamini kuwa wana hatia, kituo cha haki za binadamu cha Viasna kilisema.
Kwa sasa kuna wafungwa wa kisiasa 1,420 walioko jela nchini Belarus, akiwemo mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Ales Bialiatski. Kati ya hao, zaidi ya watu 200 ni wagonjwa sana na wanahitaji huduma ya matibabu, Viasna alisema.
Pavel Sapelka wa Viasna alisema kuwa “kadhaa, sio mamia” ya wafungwa wa kisiasa waliachiliwa kufuatia tangazo la Lukashenko la Julai 3 na kupendekeza kwamba viongozi tayari wamejaza seli tupu za jela na wafungwa wapya wa kisiasa.
Lukasjenko amekandamiza upinzani na vyombo vya habari huru tangu aingie madarakani mwaka 1994. Matokeo yaliyokuwa yakibishaniwa ya uchaguzi wa urais wa 2020 yalimruhusu kushinda muhula wa sita na kuzua maandamano ambayo yalikuwa makubwa na marefu zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Wenye mamlaka walijibu kwa ukali, na kuwakamata watu wapatao 35,000; viongozi wengi mashuhuri wa upinzani walifungwa jela na wengine kukimbia nchi.
Wanaharakati wanasema mamlaka imeweka mazingira sawa na mateso katika magereza, kuwanyima wafungwa wa kisiasa huduma ya matibabu, uhamisho na mikutano na wanasheria na jamaa.
“Licha ya hali mbaya ya kufungwa gerezani, baadhi ya Wabelarusi maarufu hawakukubali hatia, hawakutubu hadharani na kumwomba Lukasjenko huruma,” Sapelka alisema.