Manchester United wanapanga kumsajili mshambuliaji wa Paris Saint-Germain Xavi Simons, jambo ambalo linaweza kuwafanya wachezaji watatu wa kimataifa wa Uholanzi kusajiliwa na klabu hiyo msimu huu wa joto, linasema The Sun.
United wanakaribia kukamilisha uhamisho wa Euro milioni 42.5 kwa mshambuliaji Joshua Zirkzee, ambaye tayari amekubali kujiunga nao kutoka Bologna ya Italia, huku pia wapo kwenye mazungumzo na Bayern Munich kuhusu uhamisho wa euro milioni 50 kwa ajili ya beki Matthijs de Ligt.
Inaripotiwa kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ana nia ya kuhamia United, huku Bayern wakifahamu nia yake ya kutaka kuondoka na kujiunga na Mashetani Wekundu. Hata hivyo, wakati mazungumzo kati ya klabu hizo mbili yakiendelea, bado hakuna makubaliano.
Simons, 21, amefanya vyema kwenye michuano ya Euro 2024 na amekuwa na muda mzuri kwa mkopo katika klabu ya RB Leipzig msimu uliopita ambapo alifunga mabao 10 na kutoa asisti 15 katika michezo 43.
PSG ililipa €12m kwa PSV Eindhoven ili kumsajili tena mwaka wa 2023, kabla ya kumpeleka nje kwa mkopo, na sasa wanaweza kutafuta kurudisha €70m kutokana na uhamisho wa kudumu huku United, Leipzig na Bayern zikimfuatilia.