Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amependekeza Serikali ifanye mapitio ya kina ya mgawanyo wa bajeti kwa ajili ya posho za mazingira magumu kwa Maofisa wa Magereza na kuboesha bajeti kuhakikisha ustawi wa Maofisa wa Magereza.
Kupitia Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, CAG amesema “Kanuni ya 46(1) ya Kanuni za Utumishi wa Magereza ya Mwaka 1997 inawataka Maofisa Magereza wote wawe na haki ya kupata posho ya mazingira magumu, usafiri, na posho ya kazi za usiku”
“Wakati wa ukaguzi wangu nilibaini kuwa Idara ya Jeshi la Magereza (Fungu 29) ilitenga bajeti ya Sh. bilioni 18.25 kwa ajili ya posho ya mazingira magumu, ambayo ni sawa na asilimia 15 ya mshahara, hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2022/23, Maofisa wa Magereza hawakulipwa posho zao za mazingira magumu kutokana na kutopewa fedha kutoka Hazina, kutolipwa kwa posho za mazingira magumu kwa Maofisa wa Magereza kunaweza kuathiri ari ya ufanyaji kazi na ustawi wao”