Mapacha wachanga waliripotiwa kuuawa katika mlipuko wa Israeli huko Gaza wakati baba yao alikuwa katika ofisi ya serikali ya mitaa kuandikisha kuzaliwa kwao.
Asser, mvulana, na Ayssel, msichana, walikuwa na umri wa siku nne tu wakati baba yao Mohammed Abu al-Qumsan alipokwenda kuchukua vyeti vyao vya kuzaliwa.
Akiwa mbali, majirani zake walipiga simu kusema nyumba yao huko Deir al Balah ilikuwa imelipuliwa.
Mlipuko huo pia uliua mkewe na bibi wa mapacha hao.
“Sijui kilichotokea,” alisema. “Nimeambiwa ni bomu ambalo liligonga nyumba yangu.”
“Sikuwa na wakati wa kuwasherehekea wanangu,” aliongeza.
Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema watoto wachanga 115 wamezaliwa na kisha kuuawa wakati wa vita mpaka hivi sasa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, familia hiyo ilifuata amri ya kuuhamisha mji wa Gaza katika wiki za mwanzo za vita vya Israel na Gaza, kutafuta hifadhi katikati mwa ukanda huo, kama jeshi la Israel lilivyoagiza.
Israel inasema inajaribu kuepuka kuwadhuru raia na inalaumu vifo vyao kwa Hamas wanaoendesha shughuli zao katika maeneo yenye makazi ya watu wengi, ikiwa ni pamoja na kutumia majengo ya kiraia kama makazi.
Makaazi kadhaa ya aina hiyo huko Gaza yameshambuliwa katika wiki chache zilizopita.