Watu zaidi ya 50 wameripotiwa kuuawa katika mapigano makali baina ya askari wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi moja la wanamgambo magharibi mwa nchi.
Stanys Liby, Chifu wa kijiji jirani na eneo la tukio cha Kikomo, aliiambia tovuti ya habari ya ‘Media Congo’ jana Jumatatu kuwa, mapigano hayo ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa Mobondo yametokea katika kijiji cha Kinsele eneo la Kwamouth, mkoa wa Mai-Ndombe, kaskazini mashariki mwa mji mkuu, Kinshasa.
Ameongeza kuwa, wanajeshi 9 na wapiganaji 41 wa kundi la wanamgambo wa Mobondo wameuawa katika makabiliano hayo ya Jumamosi. Naye Mbunge wa eneo la Kwamouth, David Bisaka sambamba na kuthibitisha idadi ya waliouawa katika mapigano hayo, amesema miili ya wahanga hao imepelekewa katika hifadhi mbali mbali za maiti jijini Kinshasa.
Mwezi uliopita, mashambulizi mabaya yanayohusishwa na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) yalisababisha vifo vya takriban raia 50 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo .
Haya yanajiri huku Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kikisema huenda kikalazimika kuakhirisha mpango wa kuwaondoa wanajeshi wake katika mkoa unaokumbwa na vita wa Kivu Kaskazini kutokana na kuwepo kwa askari wa Rwanda mashariki mwa DRC.