Mapigano yamekuwa yakiendelea huko Masisi kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokeasia ya Kongo (DRC).
Madaktari Katika mji wa Bambo ulio Kilomita 60 karibu na mji wenye wakazi wengi wa Goma wamethibitisha vifo vya watu watano na wengine 30 kujeruhiwa katika mapigano hayo.
Mapigano hayo yamehusisha matumizi ya silaha nzito na nyepesi pamoja na kupeleka ndege za kivita aina ya Sukhoi 25.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Stephane Dujarric amethibitisha kuwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Congo MONUSCO na wanajeshi wa DRC FARDC wameungana na kuanzisha operesheni, (Springbok).
Alisema “Wenzetu wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanatuambia kwamba wameanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa Kongo huko Kivu Kaskazini ili kulinda miji muhimu ya kikanda ya Goma na Sake.
Operesheni Springbok – kama inavyoitwa – inafanywa ili kukabiliana na mapigano yanayoendelea kati ya wanamgambo wa M23 na makundi yenye silaha katika jimbo hilo pamoja na ghasia yaliyofanywa na M23 kuelekea Sake.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa Kongo wanashika doria katika maeneo muhimu ili kulinda watu na kuzuia ghasia zinazofanywa na M23.