Watu 18, wakiwemo wanajeshi wanane, waliuawa katika mashambulizi ya kundi lenye silaha magharibi mwa Sudan Kusini siku ya Jumatatu, kaimu gavana wa jimbo hilo ameliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumanne.
“Nane kati yao ni wanajeshi na kumi ni raia.
Ilikuwa asubuhi (ya Jumatatu) ambapo washambuliaji walishambulia kituo cha polisi” huko Tharkueng Payam, kaimu gavana wa jimbo la Bahr el Ghazal Magharibi, Arkenjelo Anyar Anyar ameliambia shirika la habari la AFP. Miongoni mwa raia waliouawa, “ni watoto, wanawake, wazee. Walichomwa moto kwa sababu hawakuweza kukimbia,” gavana amebaini. Ameongeza kuwa zaidi ya watu 2,000 wamekimbia makazi yao.
Kulingana na Arkenjelo Anyar Anyar, “vijana wenye silaha” kutoka jimbo jirani la Warrap walichoma moto soko, nyumba na kituo cha polisi kutokana na mzozo wa ardhi. “Hali sasa imedhibitiwa,” naibu gavana amesema.
Siku ya Jumatano, takriban watu 39 waliuawa na wengine 53 kujeruhiwa katika mapigano kati ya makundi mawili ya wafugaji kutoka majimbo jirani katikati mwa nchi. Kati ya mwisho wa mwezi wa Januari na mwanzoni mwa mwezi wa Februari, takriban watu 73 waliuawa katika mashambulizi ya kikabila kati ya Ngok na Twic, matawi mawili ya kabila la Dinka, ambalo ni kubwa zaidi nchini, katika mkoa wa Abyei, eneo la mpaka linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini.
Tazama pia…..