Ndoa ya Dr. Juma Mwaka Juma na Mkewe Queen Oscar Masanja haijavunjika, limesema Baraza la Ulamaa lililokutana kwa dharura leo Jijini Dar es salaam ikiwa ni siku chache toka Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam atangaze kuvunjika kwa Ndoa hiyo.
Taarifa ya Baraza hilo kwa Vyombo vya Habari leo imesema baada ya kuliangalia kwa kina swala la Ndoa hiyo limefikia maazimio ya mambo manne ambapo moja ni kuwa Ndoa hiyo haijavunjika hivyo kwa kuwa kuna malalamiko yaliyopelekwa katika ofisi ya Qadhi, malalamiko hayo au kesi hiyo iendelee katika ofisi ya Qadhi na Baraza la Ulamaa litafuatilia kwa karibu kinachoendelea.
Azimio la pili la Baraza hilo ni kuwafahamisha Waislamu popote pale walipo wasisite kufanya mawasiliano na Baraza la Ulamaa popote pale watakapoona kuna upindishwaji wa mambo huku azimio la tatu likiwa kuwakumbusha kuwa Muhimili wa Mahakama ya Qadhi ni Muhimili muhimu na ungojitegemea hivyo sio sahihi maamuzi yake kuingiliwa na Mamlaka za BAKWATA Wilaya au Mkoa, na pale suala litakaposhindikana katika Mahakama ya chini suala hilo litapanda katika ngazi ya juu ndani ya Muhimili huo na si vinginevyo.