Leo March 27 Wakazi wa Mkoa wa Mara wamejitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Mkoa huo John Tupa ambaye alifariki kifo cha ghafla akiwa katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Tarime.
Marehemu John Tupa enzi za uhai wake.
Marehemu Tupa alikutwa na mauti hayo asubuhi ya March 25 akiwa kwenye shughuli za kikazi wilayani Tarime na kusemekana Tupa alianguka ghafla na kuanza kutokwa povu akiwa katika ofisi za DC wa Tarime John Henjewele.
Baada ya kutokea hali hiyo alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime na ilipofika saa 4.30 asubuhi madaktari walithibitisha kuwa amefariki dunia na kabla ya kukumbwa na umauti, Tupa alikuwa akipokea taarifa ya wilaya kutoka kwa Henjewele.
Marehemu John Gabriel Tupa alizaliwa Januari mosi 1950 na amewahi kuwa mwalimu na kushika nyadhifa mbalimbali kama mkuu wa wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma na aliwahi kufanya kazi kama msaidizi wa ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, taratibu za mazishi zinaandaliwa kwa kushirikiana na familia ya marehemu, ofisi ya mkuu wa mkoa na ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).