Maradhi ya kipindupindu yanaelezwa kuyatesa mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi kutokana na kuongezeka idadi ya wagonjwa wa maradhi hayo.
Serikali kadhaa za Afrika Magharibi zinajaribu kudhibiti mlipuko wa kipindupindu, ikiwa ni pamoja na Nigeria ambapo afisa wa ngazi ya juu wa afya amesema kwamba, mamilioni ya watu wanapewa chanjo ili kufidia mapengo makubwa ya kinga dhidi ya ugonjwa huo.
Takriban watu 573 kati ya 11,640 walioambukizwa kipindupindu nchini Nigeria, wamekufa tangu mlipuko wa sasa uanze Desemba mwaka jana (2022), ingawa maafisa wanakadiria kwamba, idadi hiyo ambayo sasa inapungua kwa sababu ya juhudi za matibabu inaweza kuwa kubwa zaidi katika majimbo ambayo hayawezi kugundua maambukizo mengi.
Nchini Niger, watu 37 wamefariki dunia katika kesi 865 kufikia Oktoba, wakati Guinea imeripoti vifo 58 kati ya maambukizi 497 tangu kuzuka kwa ugonjwa huo mwezi Juni mwaka huu.
Cameroon pia ni taifa jingine la Afrika Magharibi ambalo linasumbuliwa na maradhi ya kipindupindu.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa, idadi ya visa vilivyorekodiwa vya maambukizo ya kipindupindu kote ulimwenguni vimeongezeka mara mbili.
Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa kuna visa kati ya 1,300,000 na 4,000,000 vya kipindupindu duniani kila mwaka, na takriban watu 143,000 hufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.