Marekani imesema kuwa haihimizi wala kuwezesha mashambulizi ndani ya Urusi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema baada ya mamlaka ya Urusi kusema kwamba walidungua ndege zisizo na rubani ambazo zilijaribu kushambulia Moscow mapema Jumatano, Reuters limeripoti.
Ni juu ya Ukraine kuamua jinsi itakavyochagua kujilinda kutokana na uvamizi wa Urusi ulioanza Februari mwaka jana, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema, akiongeza kwamba Urusi inaweza kumaliza vita wakati wowote kwa kujiondoa Ukraine.
Mashambulio ya ndege zisizo na rubani ndani kabisa ya Urusi yameongezeka tangu ndege mbili zisizokuwa na rubani kuharibiwa kwenye Ikulu ya Kremlin mapema Mei.
Mashambulio ya ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Urusi yamezidi kuwa ya kawaida katika miezi ya hivi karibuni.
Marekani, ambayo imeipatia Ukraine msaada mkubwa wa silaha na zana nyingine za kijeshi ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi, imekuwa ikisema haiungi mkono mashambulizi ndani ya Urusi.