Ikulu ya White House mjini Washington imesema Marekani inatarajia shirika la nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi, OPEC pamoja na washirika wao, wataongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta baada ya rais Joe Biden kufanya ziara Mashariki ya Kati wiki iliyopita.
Hata hivyo, msemaji wa ikulu hiyo Karine Jean-Pierre amesema katika mkutano na waandishi wa habari, kuwa hilo litategemea ridhaa ya OPEC na washirika wake, na yumkini matokeo yatadhihirika katika muda wa majuma mawili.
Utawala wa Biden unakabiliwa na shinikizo kubwa kuutaka ushushe bei ya mafuta na bidhaa nyingine, wakati uchaguzi wa katikati ya muhula wa tarehe 8 Novemba ukikaribia.
Kufuatia vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi baada ya nchi hiyo kuivamia Ukraine, bei ya pipa la mafuta ghafi ilipanda hadi dola 139 mwezi Machi, ikiwa bei ya juu zaidi kurikodiwa tangu mwaka 2008.