Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, kutoka chama cha Republican, Kevin McCarthy, ameondolewa kwenye wadhifa wake wakati wa kura ya kihistoria katika Congress, kufuatia malumbano ya ndani ya chama chake.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Bunge la Marekani: Spika wa Baraza la Wawakilishi, kutoka chama cha Republican, Kevin McCarthy, ametimuliwa kwenye wadhifa wake Jumanne, Oktoba 3, baada ya mabishano makali kati ya wahafidhina ndani ya taasisi hiyo. Wabunge 216 waliochaguliwa walipiga kura ya kumfukuza, wakiwemo wanane wa Republican, dhidi ya 210.
Kura hii inafungua kipindi cha msukosuko mkali katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, ambapo mtu mwingine lazima achaguliwe. Jioni, Rais Joe Biden alitoa wito kwa wawakilishi waliochaguliwa wa Baraza hilo kumchagua haraka kiongozi mpya, katika kukabiliana na “changamoto za dharura” zinazoikabili Marekani. “Kwa vile changamoto za dharura za nchi yetu haziwezi kusubiri, Rais anatumai kuwa Ikulu itamchagua kiongozi mpya,” Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre amesema katika taarifa.
Kevin McCarthy amefukuzwa katika uasi wa mrengo wa kulia – mara ya kwanza kabisa kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kupoteza kura ya kutokuwa na imani naye.
Matokeo ya mwisho yalikuwa 216-210 kumng’oa mbunge wa California kama kiongozi wa walio wengi wa chama cha Republican katika baraza la chini la Congress.