Marekani imesitisha uwasilishaji wa mabomu kwa Israel kutokana na wasiwasi kwamba ilikuwa inapanga kufanya mashambulizi makali katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza.
Kulingana na afisa mkuu wa Marekani, shehena hiyo ilijumuisha mabomu 1,800 ya pauni 2,000 na mabomu 1,700 ya pauni 500.
Afisa huyo, ambaye aliomba kutotajwa jina, mnamo Jumanne (Mei 7) alisema kuwa Marekani ilikuwa na wasiwasi hasa kuhusu vilipuzi hivyo vikubwa na jinsi ambavyo vinaweza kutumika katika eneo la mijini lenye watu wengi.
Zaidi ya raia milioni moja kwa sasa wamejihifadhi Rafah baada ya kulazimika kuhama maeneo mengine ya Gaza kutokana na mzozo wa Israel na Hamas.
Kihistoria Marekani imetoa kiasi kikubwa cha misaada ya kijeshi kwa Israel.
Hilo limeongezeka tu baada ya shambulio la Hamas Oktoba 7 lililoua takriban 1,200 nchini Israel na kupelekea takriban 250 kuchukuliwa mateka na wanamgambo hao.