Balozi mpya wa Marekani hivi karibuni atatua Niger kushiriki katika juhudi za kidiplomasia zinazolenga kurejesha serikali halali, iliyopinduliwa na wanajeshi, Washington imesema.
Mwanadiplomasia Kathleen FitzGibbon aliidhinishwa na Bunge la Seneti mnamo Julai 27, siku moja baada ya jeshi kuchukua mamlaka. Alikuwa akisubiri kurasimishwa kwa uteuzi wake kwa karibu mwaka mmoja, kutokana na vita vya kisiasa vilivyomlenga yeye mwenyewe.
“Tunafanya kinachowezekana ili Balozi FitzGibbon awasili katika mji mkuu wa Niger, Niamey,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Vedant Patel amewaambia waandishi wa habari.
Amehakikisha kwamba kuwasili huku hakumaanishi kwamba Marekani inaidhinisha mapinduzi ya kijeshi na kwamba Washington bado inataka kuachiliwa huru na kurejea madarakani kwa rais mteule Mohamed Bazoum.
“Hii si ishara ya mabadiliko katika sera ya Marekani, lakini kuhusika kwake kunaendelea” katika mgogoro huu, amesema.