Marekani imetishia kukatisha utoaji wa msaada wa kijeshi kwa Israeli iwapo haitochukua hatua za kuhakikisha kwamba misaada ya kibinadamu inaendelea kuingia kama inavyostahili katika ukanda wa Gaza
Onyo la Washington limetajwa kuwa lenye uzito zaidi tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Israeli na wapiganaji wa Hamas mwaka uliopita.
Aidha onyo hilo pia limejiri baada ya Umoja wa Mataifa kufanya tathimini wikendi iliopita na kubaini kwamba hakuna misaada mipya ya kibinadamu imeingia katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha wiki mbili.
Washington katika onyo lake imeitaka Israeli kuhakikisha kwamba misaada ya kutosha inawasilishwa katika Ukanda wa Gaza kuwasaidia raia walioathirika na mapigano katika kipindi cha siku 30.
Iwapo Israeli haitofanya hivyo, huenda ikapoteza msaada wa kijeshi wa mabilioni ya fedha kutoka kwa Marekani.