Ni February 28, 2024 ambapo Mapitio ya mpango mkakati wa Sekta ya Afya ya Tano (MTR HSSP V) yanatarajiwa kutolewa na Balozi za nchi ya Uswisi pamoja na Ireland kupitia Shirika la Afya Duniani WHO nchini Tanzania Tsh. Milioni 258 ili kusaidia utekelezaji wa kuboresha sekta ya Afya nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya maridhiano ya uwekwaji saini Dkt.Charles Sagoe Moses mwakilishi wa Tanzania wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema Mapitio ya mpango wa (HSSP V) yatatathmini na kuonyesha maendeleo yaliyopatikana na mambo tuliyojifunza miaka miwili iliyopita kutokana kuanzishwa kwake.
Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya ya Tano (MTR HSSP V) ndio mfumo elekezi wa upangaji wa kina na utekelezaji wa harakati za wadau wa sekta ya afya katika ngazi zote zilizoandaliwa na Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007, Dira ya 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/22 mpaka mwaka 2025/26.
Amesema mapitio hayo ni muhimu kwa kuwa yatatoa fursa kwa mpango unaofuata wa kuzingatia ujumuishaji wa changamoto na vitisho vya kiafya vinavyojitokeza kama vile ukuaji wa viwanda, ukuaji wa miji na harakati za kibinadamu zinazosababisha kuenea kwa Magonjwa.
“Serikali ya Tanzania katika miongo miwili iliyopita imepiga hatua kubwa kuimarisha mfumo wa afya kupitia mpango mkakati wa afya. Zoezi la mapitio haya ni wakati muafaka wa kuhakikisha kuwa vipaumbele vyote vya afya vinapewa umuhimu zaidi,”- alisema Dkt.Charles Sagoe Moses
Aidha Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Ireland Mhe. Mary Mcarthy alipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) huku akisema ulifanyika hivi karibuni wa Viashiria vya Idadi ya Watu, Afya na Malaria umepata mafanikio makubwa katika viashiria vya afya ikiwa ni pamoja na kupungua kwa vifo vya uzazi, vifo vya watoto chini ya miaka mitano na udhibiti wa Magonjwa ya kuambukiza.