Zaidi ya maroli 25 ambayo yanasafirisha bidhaa mbalimbali kutoka kiwanda cha karatasi Mgololo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa yamekwamba kwa zaidi ya siku tano katika kijiji cha Nyamande na Kitandiliko halmashauri ya mji wa Makambako wilayani Njombe kutokana na ubovu wa barabara katika eneo hilo.
Madereva wa magari hayo wamesema changamoto kubwa katika eneo hilo ni wakala wa barabara kuweka kifusi chenye tope na kusababisha magari kukwama hasa katika kipindi hiki ambacho mvua inanyesha na kuiomba serikali kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami ama changarawe kwani imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi.
Aidha madereha hao wamesema kutokana na adha hiyo kumesababisha watumie gharama kubwa kwaajili ya kupata chakula na kueleza kuwa mpaka sasa hakuna kiongozi wa serikali ambaye amefika katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kitandililo akiwemo Obedi Msingwa wamesema kutokana na barabara hiyo kutopitaka kwa zaidi ya siku tano kumesababisha abiria wanaotoka mufindi kuishia Kitandililo na kutafuta gari lingine huku wanaotoka Makambako wakiishia Nyamande,ambapo wanalazimika kutembea umbari wa kilomita moja kuyafikia magari hayo.
Diwani wa kata ya kitandililo Imani Fute amekiri kutokea kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa barabara hiyo ipo chini ya wakala wa barabara (Tanroad) Iringa na kufafanua jitihada za kutatua adha hiyo zinaendelea kwa kuwasiliana na viongozi wa wakala wa barabara na mbunge wa jimbo la mufindi.
Naye meneja wa Tanroad mkoa wa Iringa Yudas Msangi amekiri kupokea changamoto hiyo na kueleza kuwa hali hiyo imesababishwa na mvua ambazo zinaendelea kunyesha na kufafanua kuwa wataifanyia marekebisho pindi mvua zikipungua huku akiweka mpango wa kuifanyia usanifu barabara hiyo na kuiombea fedha ili ijengwa kwa kikiwango cha lami kwa miaka ijayo.
“Lakini tutafanya tunavyoweza ili paweze kupitika na tunaenda kufanya upembuzi yakinifu ili baadaye huko fedha ikipatikana tuweze kujenga kwa kiwango cha lami lakini sio mpango wa leo au kesho”