Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limetolea ufafanuzi wa taarifa ya aliyekuwa akifanya kazi ya udereva katika kampuni ya ASAS Martin Chacha aliyefikwa na umauti akiwa gerezani baada ya kuugua ghafla wakati akitumikia kifungo , tofauti na taarifa za awali zilizosambaa mitandaoni zikisema mtu huyo aliuawa kwa kipigo baada ya kuiba mafuta .
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa ,ACP Allan Bukumbi amesema Martin Chacha alikutwa na hatia ya kuiba mafuta aina ya Dizeli Lita 383 mali ya kampuni ya ASAS aliyokuwa akiifanyia kazi na alihukumiwa kifungo cha miezi 3 jela.
Hata hivyo Kamanda Bukumbi amesema mnamo Tarehe 28 February 2024 Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa lilipokea taarifa kutoka kwa mkuu wa Gereza la Mkoa wa Iringa kuhusu kifo cha mfungwa mwenye namba ya utambulisho 47/2024 aitwaye Martin Mwita Chacha 46 ambaye pia ni mkazi wa kunduchi Dar es Salaam .
Martin Chacha alifariki katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa wakati akipewa matibabu baada ya kuugua ghafla alipopatwa maumivu makali upande wa moyo
Na kulalamika kwa wafungwa wenzake waliokuwa nae katika shughuli za kilimo eneo la gereza la Mlolo na kukimbizwa hospitali haraka.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ukisubiri taratibu za kitaalamu kufanyika iki kubainu tatizo la kifo chake cha ghafla.