Serikali ya Tanzania imesema kuanzia sasa hakutokuwa tena na biashara ya usafirishaji wa Wanyama pori hai nje ya nchi kwa ajili ya shughuli za kibiashara kama ilivyokuwa hapo awali, hii ni ili kulinda rasimali zilizopo kwa kuhakikisha zinaedelea kuchangia uchumi wa Nchi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja ameyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizosambaa kwamba biashara ya Wanyama pori hai imerejea tena nchini Tanzania.
Amesisitiza kuwa Wanyamapori hai watakaoruhusiwa kutoka nje ya nchi ni wale tu watakaohusika na shughuli za utafiti wa kisayansi ambapo Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) ina mamlaka ya kuidhinisha wanyamapori kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi kwa shughuli za utafiti wa kisayansi baada ya kupokea maombi.
‘’Mamlaka ya nchi huwa inaamua aina na idadi ya wanyama itakayotoa kama zawadi lakini kwa kuzingatia mikataba ya Kimataifa tuliyoridhia kama nchi mfano ni zawadi ya ndege aina ya Tausi iliyotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Kenya na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli’´Amesisitiza Mhe. Mary Masanja.