Daktari wa klabu ya Chelsea Eva Carneiro amewashukuru masabiki wa klabu hiyo ambao walichukua muda wao na kutuma ujumbe wa kumuunga mkono baada ya kocha wa klabu hiyo Jose Mourinho kumshutumu kufuatia tukio lililojitokeza kwneye mchezo wa kwanza wa ligi kuu ya England kwa mabingwa hao dhidi ya Swansea.
Huku matokeo yakienda kinyume na matarajio ya kocha huyo kwenye mchezo huo dhidi ya Swansea ambako Chelsea walibanwa na kutoka sare ya 2-2, Mourinho alimshutumu daktari wa timu baada ya kitendo cha kwenda kumtibu Eden Hazard wakiwa akiwa ameumia .
Mourinho alisema kuwa Daktari huyo alikosea kwa alichofanya kwani kwenda kumtibu kiungo Eden Hazard kuliifanya timu yake ibaki na wachezaji nane uwanjani hali ambayo iliwafanya wacheze kwa mazingira magumu .
Wakati kitendo hicho kinatokea Chelsea ilikuwa imebaki na wachezaji 9 uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kipa Thibaut Courtois na daktari huyo kwenda kumtibu Hazard ambaye sheria zinalazimu mchezaji kutoka nje kabla ya kurudishwa uwanjani kwa ruhusa ya refa kuliifanya Chelsea kubaki na watu 8 tu kwa takribani dakika mbili.
Mourinho alimshutumu daktari huyo kwa kusema kuwa baadhi ya watu wanaokaa kwenye benchi la ufundi wanapaswa kuelewa jinsi ambavyo mchezo wa soka unakwenda huku akiongeza kuwa Hazard hakuwa ameumia alikuwa amechoka na alihitaji kuachwa na angenyanyuka mwenyewe.
Watu wengi wametafsiri tukio hili kama dharau toka kwa Mourinho na wamekuwa wakimtumia daktari huyo ujumbe wa kumuunga mkono ktiando ambacho kimemgusa daktari huyo ambaye amejijengea umaarufu mkubwa akiwa daktari pekee wa kike kwenye timu kubwa.