Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hadi kufikia March 15, 2022 watu 33,789 wamethibitika kuwa na UVIKO – 19 na watu 803 wamepoteza maisha nchini.
Kwa upande wa uchanjaji watu 2,820,545 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, wamepata chanjo kamili dhidi ya ugonjwa huo idadi ambayo ni sawa na asilimia 9.17 ya watanzania 30,740,928.
Akizungumza wakati akitoa tamko kuhusu hali ya Uviko-19 kwa miaka miwili baada ya ugonjwa huo kuingia nchini, Waziri Ummy amesema Serikali imelegeza masharti kwa wasafiri wanaoingia nchini ambao wamekamilisha dozi ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
Hiyo inamaanisha kuwa hata Watanzania waliokwisha chanja hawatalazimika kushughulikia vipimo ikiwa watakuwa na safari za kurudi nchini.
Kuanzia kesho Machi 17, 2022 wasafiri hao wanaondolewa hitaji la kuwa na cheti cha kipimo cha kuthibitisha kutokuwa na maambukizi (negative RT – PCR certifícate) kilichokuwa kikihitajika hapo awali.
“Serikali inaimarisha huduma za ukaguzi na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini katika maeneo ya viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu kwa kuzingatia hali ya sasa ya maambukizi ya Uviko-19 nchini na mwenendo wa ugonjwa huu duniani” Ummy Mwalimu
“Haya na masharti mengine yataainishwa kwenye mwongozo wa wasafiri ambao utakua ukibadilika kulingana na mwenendo wa maambukizi ya ugonjwa huu nchini na duniani kwa ujumla,” amesema Ummy Mwalimu.
“Tutahamasisha wananchi kupata chanjo dhidi ya Uviko-19. Ninawahimiza wananchi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kupata chanjo kwa kuwa chanjo ndio nguzo kuu kwa sasa katika kujikinga na kukabiliana naugonjwa huu,” Ummy Mwalimu