Watumishi sita wa kituo cha afya cha Njombe Mjini wamekamatwa na Polisi Mkoani Njombe kwa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka ili kutoa maelezo kutokana na upotevu wa vifaa vya kituo hicho cha afya vyenye thamani ya Tsh. milioni 15 ikiwemo mashine ya kupima mkojo.
Mtaka ametoa maagizo hayo baada ya kushtukiza kwenye kituo hicho cha afya akiwa na taarifa ya upotevu huo ambapo pia ameagiza Mganga Mkuu wa Mkoa huo kufanya ukaguzi mkali kwenye zahanati, vituo vya afya na Hospitali zote za mkoa huo huku pia akimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Kuruthum Sadick kuwasimamisha kazi Watuhumiwa wote ili kupisha uchunguzi.
“Tunafedhehesha taaluma zetu kwahiyo niombe RMO ufanyike ukaguzi wa vituo vyote vya afya, tuangalie vifaa tulivyopokea, utokaji wake na ambavyo vimetumika”
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Juma Mfanga, amesema miongoni mwa mashine zilizoripotiwa kupotea ni pamoja na mashine ya kupima mkojo, box 91 za vipimo vya kupima HIV, box 51 za vipimo vya kupima Malaria pamoja na box 48 za vitendanishi kwa ajili ya kupima uwingi wa damu huku RPC wa Njombe Mahamoud Banga akithibitisha kuwashikilia Watumishi sita wa kituo hicho kwa ajili ya uchunguzi.