Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah amesema Basi la Kampuni ya MOA ambalo leo lilitumbukia majini likiwa linatoka ndani ya kivuko kwenda Nchi kavu Pangani, tayari limetolewa kwenye maji kwa kuvutwa kwa kamba na tingatinga na kwa sasa huduma zinaendelea kama kawaida ambapo amewapa pia pole Wana Pangani na Watanzania kwa taharuki na kusema wanafuatila ili matukio kama hayo yasijirudie tena.
@AyoTV_ imeongea na Mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Naila Yusuph ambaye amesema “Nilikuwa navuka naenda Mwera tumepanda feri mpaka tumevuka tukaona gari imepanda imefika hapa ikashindwa kuvuka ikaanza kurudi nyuma, nyuma, nyuma tukaanza kupiga kelele eeh eeh jaman jaman”
Shuhuda mwingine ametoa ushauri kwa Wamiliki kuyafanyia service magari yao “Inaonekana gari haina breki za kutosha, service ni muhimu”
Kwa upande wake DC Zainab amesema “Tumepata changamoto kidogo kivuko kikiwa kinatoka Pangani Mjini wakati kinashusha abiria pamoja na kushusha magari, gari ikafeli breki na ikazama Mto Pangani, nawashukuru Wakandarasi wanaotengeneza Daraja la Mto Pangani kwa kuitikia kwa haraka katika kuitoa haraka gari kwenye Mto, tunamshukuru Mungu hakukuwa na abiria ndani ya gari, tumelitoa gari salama na huduma za kivuko zinaendelea nawapa pole Wana Pangani kwa taharuki lakini tunafuatilia ili matukio yasijirudie tena”