Usitishaji vita wa siku nne huko Gaza kati ya Israel na Hamas umeanza katika muda uliopangwa saa 7 asubuhi, ambao utafuatia kuachiliwa huru kwa wanawake na watoto 13 chini ya mapatano yaliyosimamiwa na Qatar.
Mateka wataachiliwa saa tisa baada ya kuanza kwa utulivu wa kibinadamu huko Gaza, wizara ya mambo ya nje ya Qatar ilisema.
Msaada ulioongezeka kwa Wapalestina utaanza kuingia Gaza “haraka iwezekanavyo”, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed al-Ansari aliongeza.
Hakusema ni wafungwa wangapi wa Kipalestina wataachiliwa, lakini maafisa wamesema watatu wataachiliwa kwa kila mateka.
“Kundi la kwanza la raia kuachiliwa kutoka Gaza litakuwa karibu saa kumi jioni ya siku hiyo hiyo. Watakuwa 13 kwa idadi, wote wanawake, na watoto na wale mateka wa familia moja watawekwa pamoja katika kundi moja,” aliongeza.
Inatarajiwa kwamba mateka wasiopungua 50 wataachiliwa na Hamas wakati wa usitishaji vita wa siku nne chini ya mkataba mpya na Israel, uliosimamiwa na Qatar na Marekani.
Makumi ya watoto na mama zao waliokuwa mateka huko Gaza tangu uvamizi wa kikatili wa Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba wataachiliwa huru kupitia Misri, kulingana na makubaliano.