HATIMAYE safari ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuwania tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Africa, AFCON 2015 nchini Morocco amefia mikononi mwa timu ya taifa ya Msumbiji ‘Black Mambas’.
Taifa Stars ikiwa ugenini katika dimba la Taifa la Zimpeto nje kidogo ya jiji la Maputo imetandikwa mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano wa kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya AFCON mwakani.
Katika Mechi ya kwanza iliyopigwa wiki mbili zilizopita jijini Dar es salaam, vijana wa Mholanzi, Mart Nooij walitoka sare ya mabao 2-2 na leo hii walihitaji kupata ushindi wa aina yoyote ile au sare ya kuanzia mabao 3-3.
Matokeo ya jumla baada ya mechi mbili, Msumbiji wamefanikiwa kufunga mabao 4 na Taifa stars matatu, hivyo vijana wa Nooij kutupwa nje ya michuano kwa wastani wa mabao 4-3.
Msumbiji walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kupitia kwa Josimar Tiago Machaisse, lakini Mbwana Ally Samatta akaisawazishia Stars katika dakika ya 77.
Dakika ya 83, kiungo mshambuliaji wa Msumbiji, mzoefu, mwenye ujanja mwingi wa kupiga chenga na kumiliki mpira, Elias Gasper Pelembe aliifungia ‘Domingues’ Msumbiji bao la pili na la ushindi.
Kihistoria Msumbuji wamemekuwa wababe wa Taifa Stars inapofika michezo ya mtoano, hasa kufuzu mataifa ya Afrika.
Mwaka 2007 Stars chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa mwisho jijini Dar es salaam kuwania kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana na ingeshinda ingefuzu.
Bao pekee la Msumbiji lilifungwa dakika ya za mapema kipindi cha kwanza na aliyekuwa nahodha wake, Tiko Tiko akiunganisha kwa kichwa krosi nzuri iliyochongwa kutoka winga ya kulia na Elias Pelembe.
Mwaka 2012 Taifa stars ilitolewa tena na Msumbiji kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2013 nchini Afrika kusini.
Hatua hii ilifikia baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es salaam na kupata matokeo kama hayo mjini Maputo.
Kwahiyo Msumbiji bado wameendelea kuwa wababe wa Tanzania katika michezo ya mtoano.
Poleni sana Taifa Stars, Poleni Watanzania wote. Mipango mipya inatakiwa kuwekwa.
Source:shaffihdauda.com