Matumzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yamerahisisha shughuli za kutoa huduma kwa wananchi na kuongeza ukusanyaji wa mapato yakiziba mianya ya upotevu wa mapato.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Fungo alisema “matumizi ya TEHAMA yamerahisisha sana shughuli za serikali za kutoa huduma kwa wakati na kwa urahisi kwa wananchi.
Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiwezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma upatikanaji wa fedha kwenye ujenzi na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA ikiwemo mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam ili wawe na uelewa wa kutosha kuweza kufanyia kazi mifumo, miundombinu na vifaa vya TEHAMA kwa wakati”.
Wakati huohuo, alisema kuwa halmashauri imejipambanua sana kwenye matumizi ya TEHAMA kufikisha habari kwa wananchi. “Tunahakikisha sisi wenyewe tunakuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wananchi kupitia mitandao ya kijamii. Mfano tovuti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma www.dodomacc.go.tz tumekuwa tukiweka habari na taarifa mbalimbali za maendeleo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na mrejesho kutoka kwa wananchi.
Pia tunazo kurasa za mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook na Youtube channel inayofahamika kama Dodoma City Tv” aliongeza.