Watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauwaji ya watu watatu katika matukio mawili tofauti yanayotajwa kuwa ni kulipiza kisasi katika kijiji cha Ilabilo wilayani kakonko mkoani hapa.
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Evance Malasa amemueleza Mkuu wa Mkoa Kigoma kuwa katika tukio la kwanza mtoto aliyekuwa na umri wa miaka mitano (5) mwenye ulemavu wa miguu na mikono aliyefahamika kwa jina la Simion Furaha, alipotea Alhamis ya tarehe 18 na mwili wake kukutwa siku ya Jumamosi tarehe 20, 2024 ukiwa umefukiwa katika kichaka jirani na makazi ya watu kijijini hapo huku ukiwa na ishara ya kunyongwa.
Kanali Malasa amesema kufuatia tukio hilo wananchi wenye hasira walimvamia Stephano Ndagwe ambae nyumba yake ipo jirani na eneo ulipokutwa mwili wa Simon Furaha na kuanza kumshambulia kwa vitu vyenye ncha kali na kusababisha kifo chake sambamba na kuchoma moto nyumba na kuharibu mazao yaliyokuwa shambani jirani na nyumba hiyo.
Amebainisha kuwa baada ya tukio hilo, wananchi hao wakaendelea kuwatafuta watu wengine wanaoishi katika nyumba ya marehemu Stephano na kumkamata mtoto wa marehemu aliyetambuliwa kwa jina Alfayo Stephano (14 ) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Msingi Kabingo na kumuuwa kwa kumchoma moto kwa kile wananchodai kuangamiza kizazi cha watu katili katika kijiji hicho.
Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Adengenye ametembelea kijijini hapo na kuwasihi wananchi wa kijiji hicho kuacha tabia ya kujichukulia Sheria mkononi na kuwataka watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabaini watuhumiwa wa matukio hayo na kuwafikisha mahakamani.
Aidha Andengenye amesema serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya aina hiyo na kamwe haitawaacha salama watu wanaotaka kuweka mazingira hatarishi kwa wengine na kusisitiza kuwa hatua kali zitachukuli dhidi ya wahusika ili matukio ya aina hiyo yasiweze kujirudia.
Mpaka sasa tayari watu sita wamekamatwa kijijini hapo huku jeshi la polisi likiendelea na upepelezi wake kuhusiana na tukio hilo.