Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo na Uongozi wa Klabu ya Soka ya Ajax ya Uholanzi ili itangaze vivutio vya Utalii vya Tanzania kupitia matangazo ya jezi na mbao za matangazo (billboards) uwanjani.
Dkt. Ndumbaro amebainisha hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo wakiongozwa na Bi.Tanja Dik, Afisa Mkuu wa Uwanja na Bw. Han Mouton, Mkurugenzi wa Fedha wa timu hiyo.
Katika mazungumzo yao, Dkt. Ndumbaro amewasilisha nia ya Tanzania kushirikiana na Klabu ya Ajax katika kutangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania kupitia matangazo kwenye jezi na mbao za matangazo zilizopo katika iwanja wa klabu hiyo.
“Mazungumzo yetu yameenda vizuri na viongozi hao wamepokea pendekezo na ombi letu na kuahidi kulifikisha kwenye idara husika ya biashara pia kuendeleza mawasiliano na Ubalozi wetu uliopo hapa kuangalia namna ya kutekeleza nia hii,” amesema Dkt. Ndumbaro.
Katika hatua nyingine, Mhe. Dk Ndumbaro ametembelea na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Klabu kubwa ya Golf nchini Uholanzi ya GC BurgGolf Westerpark, Zoetermeer.
Katika mazungumzo yake na Meneja mauzo na matukio, Bi. Eline Dujardin na Mkufunzi katika klabu hiyo Bw. Ronald Mos, Dk Ndumbaro amewasilisha pendekezo la Tanzania kushirikiana na klabu hiyo katika kuandaa tamasha la golf litakalofahamika kwa jina la “Mt. Kilimanjaro Open”.
Hata hivyo, pendekezo limepokelewa vizuri na viongozi wa klabu hiyo na kuahidi kuwasiliana zaidi kupitia Ubalozi ili kuangalia namna bora ya kulitekeleza.
Waziri Ndumbaro amefanya ziara hiyo ya kikazi nchini Uholanzi kwa lengo la kutafuta fursa za kutangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania nchi humo.
Aidha, Waziri Dk Ndumbaro amepata fursa ya kufanya mazungumzo na Mhe. Irene F. M. Kasyanju, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi pamoja na watumishi wa ubalozi huo.
Akizungumza na watumishi hao, Dk Ndumbaro amewaeleza mwelekeo wa Wizara katika kutangaza utalii ikiwemo uanzishwaji wa vifurushi vya wanafunzi (student package), matumizi ya utangazaji utalii kidijitali , Utangazaji kupitia michezo, vyombo vya habari , Watu maarufu wenye ushawishi duniani na Mabalozi wa hiari wa Utalii.